Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makala akimsikiliza Bibi Mawazia Kibwana , mkazi wa Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, akitoa malalamiko kwa Mbunge wake juu ya kitendo cha kubomolewa choo chake na Mwekezaji Raia wa kigeni na kuzungusha uzio uliofikia upenuni mwa makazi yake. Mbunge huyo alitembelea kitongoji hicho mwishoni mwa wiki kujionea hali halisi ya mgogoro wa ardhi uliopo kijijini hapoMbunge wa Jimbo la Mvomero, Mkoani Morogoro, Amos Makala (kushoto) akikagua uzio uliowekwa na Kampuni ya Tanbreed Poultry Limited inayomilikiwa na Mzungu aliyenunua shamba Kitogoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero na kuzua mgogoro mkubwa wa mipaka baina yake na wananchi wa eneo hilo. Anaemuongoza ni Said Ahmad mkazi wa Kinyenze
Na: Mroki Mroki, Mvomero
MBUNGE wa jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Amos Makala ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo katika Kitongoji cha Kinyenze , Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali , Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baina ya wananchi na mwekezaji wa Kigeni aliyeuziwa shamba kijijini hapo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Kijijini hapo Makala aliyeambatana na Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Majaliwa Jaffari amewataka idara ya ardhi kuchukua hatua za haraka na dharula kutatua mgogoro huo kabla ya kuibuka kwa machafuko ya uvunjifu wa amani.
“Nimejionea mwenyewe baada ya kusikia kiliochenu juu ya mwekezaji huyu, watu wa ardhi tafadhalini sana lishughulikieni suala hili haraka sana na mkae pamoja mgogoro huu umalizike upesi iwezekanavyo, ndani ya wiki moja tatizo hili liwe limemalizika”, alisema Makala.
Aidha Makala amesema tatizo hilo likiendelea ataungana na wananchi wake kufungua kesi Mahakamani ya kumpinga mwelezaji huyo na amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kutumia mamlaka waliyonayo kufika kijijini hapo wafungue uzio huo uliowekwa na mweklezaji huyo haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali, watoto kwenda shule na watu kuvuna mazao yao yanayoibiwa na walinzi wa kampuni ya Tanbreed Poultry Limited ambayo imemega mashamba yao.
“Katika hili ninaungana nanyi na Viongozi wa Mkoa na Wilaya wafike hapa wakiwa na dola na kukata uzio huu, ili wananchi muendelee na shughuli zenu za kijamii, si haki kufunga barabara mnayoitumia kwenda katika makazi yenu na mashambani, hili lisipofanyika tutatafuta mwanansheria na kufungua kesi ya Mahakamani ya kumpinga mwekezaji huyu”,alisema Mbunge Makala.
Makala pia aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuwa watulivu pasipo kufanya vurugu katika kipindi kirefu tangu kuibuka kwa mgogoro huo bila kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu licha ya kuandikiwa barua tangu mwezi Aprili mwaka huu mgogoro huo ulipoanza kushika kasi.
“Wananchi mmefanya jambo jema sana la kuheshimu mamlaka za kisheria kwa kuwa watulivu kipindi chote lakini vinginevyo hapa machafuko yangetokea maana wananchi mpo wengi kuliko hao askari wao wanaolinda hilo shamba”, alisema Makala.
Pia alisema kwa maelezo aliyoyasikia kutoka kwa baadhi ya wazee wa kijiji hicho Ally Kidunda na Said Ahmad na viongozi wa Kijiji yaliyotolewa kwaa nyakati tofauti Mwekezaji huyo ndiye mvamizi wa eneo lao na si wananchi maana hata kijiji hakimtambui kwa maana hajawahi kufika kwao.
Nae Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Jaffari alisema watalishughulikia suala hilo haraka na hasa baada ya kufika eneo la tukio na kukiri kuna mapungufu katika ramani waliyonayo.
Agosti 23, mwaka huu wananchi hao waliitaka serikali kuingilia kati mgogoro huo haraka kabla ya machafuko kutokea wakati wakiwa katika mkutano wa hadhara uliokuwa uhudhuriwe na Mkurugenzi wa Wilaya na Maofisa wa Ardhi.
Mwisho.